1 Kisha Roho alimwongoza Yesu mpaka jangwani ili ajaribiwe na Ibilisi.

2 Akafunga siku arubaini mchana na usiku, na mwishowe akaona njaa.

3 Basi, mshawishi akamjia, akamwambia, "Ikiwa wewe ni Mwana wa Mungu, amuru mawe haya yawe mikate."

4 Yesu akamjibu, "Imeandikwa katika Maandiko Matakatifu: Binadamu hataishi kwa mikate tu, ila kwa kila neno asemalo Mungu."

5 Kisha Ibilisi akamchukua mpaka Yerusalemu, mji mtakatifu, akamweka juu ya mnara wa hekalu,

6 akamwambia, "Ikiwa wewe ni Mwana wa Mungu, jitupe chini; maana imeandikwa: Mungu atawaamuru malaika wake kwa ajili yako; watakuchukua mikononi mwao, usije ukajikwaa kwenye jiwe."

7 Yesu akamwambia, "Imeandikwa pia: Usimjaribu Bwana, Mungu wako."

8 Kisha Ibilisi akamchukua mpaka juu ya mlima mrefu, akamwonyesha falme zote za ulimwengu na fahari zake,

9 akamwambia, "Hivi vyote nitakupa kama tu ukipiga magoti na kuniabudu."

10 Hapo, Yesu akamwambia, "Nenda zako Shetani! Imeandikwa: Utamwabudu Bwana Mungu wako na kumtumikia yeye peke yake."

11 Basi, Ibilisi akamwacha, na malaika wakaja, wakamhudumia.