3 naye Yesu akawaambia mambo mengi kwa mifano. "Sikilizeni! Mpanzi alikwenda kupanda mbegu.

4 Alipokuwa akipanda, nyingine zilianguka njiani, ndege wakaja wakazila.

5 Nyingine zilianguka penye mawe pasipokuwa na udongo mwingi. Zikaota mara kwa kuwa udongo haukuwa na kina.

6 Jua lilipochomoza, zilichomeka; na kwa kuwa mizizi yake haikuwa na nguvu, zikanyauka.

7 Nyingine zilianguka kwenye miti ya miiba, nayo ikakua na kuzisonga.

8 Lakini nyingine zilianguka penye udongo mzuri, zikaota, zikazaa: nyingine punje mia moja, nyingine sitini na nyingine thelathini.

9 Mwenye masikio na asikie!"